Tuesday, April 12, 2011

Kuchakachua

Neno kuchakachua si geni katika lugha ya kiswahili. Limekuwepo kwa muda mrefu tu, ila matumizi yake yamekuwa makubwa katika siku za karibuni. Aidha kama kawaida ya watanzania, matumizi yasiyofaa ya neno hili pia yameibuka. Si ajabu kumsikia mtu anasema "ngoja nikachakachue kidogo" akiwa na maana anaenda kula. Au nimeshasikia kijana akisema "yule binti mi nishachakachua" Sijui alikua ana maana gani lakini mazingira ya mazungumzo yaliashiria matumizi mabaya ya neno kuchakachua.

Kwa kutumia neno hili tujadili namna nchi yetu inavyoharibika kutokana na kuchakachua kila kitu. Uchakachuaji umeanzia ngazi za juu kabisa serikalini mpaka chini kabisa majumbani kwetu. Majumbani kwetu wafanyakazi wa ndani wanachakachua. Unakuta dada wa nyumbani ana simu ya mkononi, na muda wote anatuma sms au kuongea. Pesa za kununua vocha anapata wapi? Jibu ni kwamba anachakachua. Pesa anayopewa kununua vitu vya nyumbani ananunua nusu yake ili apate pesa ya vocha. Matokeo yake chakula, usafi na vitu vingi vya nyumbani vinakua hafifu.

Kwa ngazi ya familia madhara yake si makubwa sana, kwani ni rahisi kudhibitiwa kabla hayajawa makubwa. Lakini inapofika katika ngazi ya nchi, wananchi wanaumia. Jukumu la wananchi wote na hasa wanasiasa ni kuona kuwa viongozi wetu hawachakachui rasilimali zetu. Tukibaini wanafanya hivyo tuwatoe.

CCM kama chama kinachoongoza serikali yetu kimeshindwa kufanya kinachotakiwa kufanyika. Ni wakati mgumu kwao kwani kuendelea kuwakumbatia mafisadi wanaochakachua nchi yetu kunaweza kuwafanya watanzania wakichakachue chama chenyewe.

CCM amkeni mfanye kinachotakiwa kufanyika. Uchaguzi wa chama cha mapinduzi ni mwakani tu, tunawatazama!

Wasalaam

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...